Saturday, October 8, 2016

SHAIRI


Soma shairi hili, kisha uyajibu maswali yanayofuata:


9.   1.   Dunia yanishangaza, kwa mikiki na myujiza,

            Yajaa sana kuwaza, ama nitajiumiza,

            Kwa maovu kuigiza, nimejigeuza pweza,

            Mola naomba ya jaza, nanuia kuwa mwema.



      2.   Utu uzima wangia, masoma namalizia,

            Michezo yanizidia, rafiki wana udhia,

            Sipati wala tulia, masomo sijafalia,

            Mwenyewe najichukia, vitabu sijavishika.



      3.   Siku nazo zayoyoma, kesho nitasema nini?

            Nitanena sikusoma, nitamdanganya nani?

            Wazazi pesa wachoma, kunipeleka shuleni,

            Kwa kuwa nimebaini, heri nitie bidii.

4.        Mawi yamenizunguka, mungu wangu nibariki,

      Kujiasa ninataka, nifanye yote ya haki,

      Ningependa kuamka, utepetevu sitaki,

      Nyuma sipendi kubaki, ningependa kufaulu.



5.   Marafiki naeleza, kuwa nimeshachapuka,

      Habari nazieneza, wala msije kumaka,

      Ukweli ninawajuza, horomo nimeondoka,

      Uvivuni nimetoka, niondoeni kundini.



6    Panda nalipulizia, kwa wa hapa na wa kule,

      Nadhani nimesikia, mkazo natia shule,

      Ukunguni nasusia, nataka kusonga mbele,

      Sitaki zenu kelele, nidhamu naifwatile.



7.   Leo nisipokazana, kesho nitakula nini?

      Nitawakidhije wana? Nitakuwa mtu duni!

      Riziki takuwa sina, nitaitwa mkunguni,

      Moto najipaliani? Heri nijikuze sasa.



8.   Mtegemea cha ndugu, atakufa maskini,

      Ama atakuwa pwagu, aishie kifungoni,

      Kwa nini niote sugu, na kweli i hadharani,

      Sitajitia shimoni, nitayapenda masomo.



9.   Baibai masahibu, msipende kunighasi,

      Nitavisoma vitabu, mitihani niipasi,

      Nigeuke mahabubu, na mtu aso muasi

      Hayana ya wasiwasi, yenu nyingi hayawani.



10. Jongoo nimemtupa, na mti wake pamoja,

      Sitataka tapatapa, ninaitafuta tija,

      Nyingi pigeni malapa, hatavishwa makoja,

      Kuna siku itakuja, mtakuja kuhiliki!



Maswali:

(a)  Andika kichwa mwafaka kinachofaa kuelezea shairi hili.                        (alama 2)

 (b) Hili ni shairi la aina gani? Toa sababu zako.                                             (alama 2)

 (c) Marafiki wa mwandishi wana tabia gani?                                                (alama 4)

 (d)      Ni nini dhamira ya mtunzi?                                                                 (alama 2)

 (e) Andika ubeti wa sita kwa lugha nathari.                                                  (alama 5)

 (f) Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumiwa katika shairi

      (i)  Mikiki                          (ii)  Kuyoyoma                        (iii)  Mkunguni

      (iv)  Panda                         (v)  Sugu

No comments:

Post a Comment